Japani huenda ikalegeza zaidi udhibiti wa virusi vya korona mipakani

Serikali ya Japani inajiandaa kulegeza zaidi udhibiti wa virusi vya korona mipakani kuanzia mapema mwezi ujao.

Serikali ililegeza udhibiti wa kukabiliana na maambukizi mipakani mnamo Septemba 7, kwa kuongeza idadi ya wanaoingia nchini humo kwa siku hadi 50,000 kutoka 20,000. Pia iliruhusu watalii wa kigeni kufanya safari za makundi bila waongozaji.

Aidha serikali kwa sasa inapanga kulegeza zaidi udhibiti kwani maambukizi mapya ya virusi hivyo yamekuwa yakipungua nchini humo. Kadhalika inatarajia kushuka kwa thamani ya sarafu ya yeni kutashawishi watalii wengi wa kigeni.

Serikali iko mbioni kufuta ukomo kwa wanaowasili kwa siku na kuruhusu watalii wa kigeni kuingia Japani kwa utalii binafsi.

Pia inajiandaa kurejesha msamaha wa viza ya muda mfupi kwa wageni kutoka nchi na maeneo yapatayo 70 ikiwa watakaa Japani kwa siku 90 ama chini ya hapo.

Serikali inatarajiwa kuamua lini itatekeleza hatua hizo za nyongeza za kulegeza udhibiti baada ya kuchunguza hali ya maambukizi na vigezo vingine.