Wanachama kadhaa wa IAEA waelezea mashaka kuhusu Iran

Makumi ya nchi wanachama wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA wametoa taarifa wakielezea mashaka kuhusu kukosa ushirikiano wa Iran kwenye ukaguzi wa nyenzo zisizowekwa wazi za nyuklia.

Taarifa ya pamoja ilitolewa na nchi wanachama 56 kwenye mkutano wa wajumbe wa bodi ya IAEA juzi Jumatano. Ilipendekezwa na Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na Marekani.

Nchi hizo zilisema Iran haijatoa ushirikiano kwa ukaguzi wa IAEA kufuatia ugunduzi wa nyenzo za nyuklia kwenye maeneo kadhaa ambayo hayakuwekwa wazi nchini humo mnamo mwaka 2019 na 2020.

Balozi wa Iran kwenye shirika hilo, Mohsen Naziri Asl alijibu vikali jana Alhamisi. Alisema taarifa hiyo “haikuwa yenye tija” na kila mmoja amefahamu “ina malengo ya kisiasa tu.”