IAEA yatoa wito kwa Urusi kusitisha uwepo wake katika mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia

Bodi ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA imepitisha azimio la kuitaka Urusi kusitisha uwepo wake katika mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia nchini ukraine.

Azimio hilo lilipitishwa kwa kura nyingi jana Alhamisi wakati wa mkutano unaoendelea wa wajumbe wa bodi hiyo. Mkutano huo umeanza Jumatatu wiki hii nchini Austria.

IAEA ina wajumbe wa bodi 35. Shirika la habari la Reuters lilisema Urusi na China zilipinga azimio hilo na kwamba mataifa saba ya bara la Asia na Afrika yalijizuia kupiga kura wakati wa kikao hicho kisichokuwa na waandishi wa habari.

Azimio hilo linaitaka Urusi haraka “kuacha vitendo vyote inavyofanya dhidi na katika Mtambo wa Nyuklia wa Zaporizhzhia” ili mamlaka sahihi za Ukraine ziweze kupata udhibiti kamili wa mtambo huo.

Ujumbe wa Urusi katika shirika hilo ulitoa tarifa ambayo inasema “Udhaifu wa azimio hili ni kwamba halisemi neno kuhusiana na mashambulizi mfululizo katika Mtambo wa Zaporizhzhia.” Pia inasema “Sababu ni rahisi kwamba mashambulizi hayo yanafanywa na Ukraine ambayo inaungwa mkono na kutetewa na mataifa ya Magharibi.”

IAEA imependekeza kuanzisha ukanda wa kulinda usalama karibu na vituo vya nyuklia. Pendekezo hilo linakuja baada ya mfululizo wa mashambulizi ya makombora yaliyosababisha kukatika kwa muda kwa umeme wa nje katika mtambo huo.