Mawaziri wa biashara wa G7 walaani uvamizi nchini Ukraine

Mawaziri wa biashara wa nchi saba zilizoendelea kiviwanda duniani G7 wamelaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na kuahidi kuimarisha mnyororo wa usambazaji bidhaa.

Mawaziri hao walitoa taarifa ya pamoja baada ya kumaliza mkutano wao nchini Ujerumani jana Alhamisi.

Taarifa hiyo inasema “Vita vya Urusi dhidi ya Ukraine vimeharibu uzalishaji wa kilimo, mnyororo wa ugavi na biashara, na kusababisha wasiwasi hasa kwa nchi zinazoendelea na zile zilizo nyuma kimaendeleo.”

Mawaziri hao wanasema “wamesalia kuwa imara” katika kujitolea kwao kuiwekea Urusi “vikwazo ambavyo havijawahi kushuhudiwa ili kulinda utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria.”

Aidha taarifa hiyo inasema mawaziri “wataendelea kuratibu hatua za kibiashara na uwekezaji za siku zijazo ili kusaidia juhudi za Ukraine za kurejea katika hali ya kawaida.”

Wakirejelea mzozo wa hivi karibuni ambao umeonyesha udhaifu wa kiuchumi, mawaziri hao wanasema “wataendelea kutafuta fursa mpya za kufanya kazi pamoja ili kusaidia kuimarisha mnyororo wa ugavi.”