Xi na Putin wakutana pembezoni mwa mkutano wa viongozi wakuu

Marais Xi Jinping wa China na Vladimir Putin wa Urusi wamekutana pembezoni mwa mkutano wa viongozi wakuu wa kikanda.

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa viongozi hao kukutana ana kwa ana tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake nchini Ukraine mwezi Februari.

Mwanzoni mwa mazungumzo yao, Putin alisema, “Urusi inathamini kwa kiasi kikubwa msimamo wa China wenye uwiano katika mgogoro wa Ukraine.”

Xi alimwambia Putin, “Katika kipindi cha mabadiliko makubwa duniani, na katika historia, China itafanya kazi na Urusi ili kutumia uongozi kama taifa rafiki lenye nguvu kubwa.”

Putin alisema Urusi inaunga mkono kwa dhati sera ya “China-moja.” Aliituhumu Marekani na washirika wake kwa kufanya vitendo vya kichokozi katika Mlango Bahari wa Taiwan.

Xi na Putin wanahudhuria mkutano wa siku mbili wa viongozi wakuu wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai. Mkutano huo ulianza jana Alhamisi nchini Uzbekistan.

Hii ilikuwa ziara ya kwanza ya Xi nje ya nchi katika kipindi cha miaka miwili na nusu. Anajiandaa kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa Chama cha Kikomunisti utakaofanyika mwezi ujao, ambapo anatarajiwa kuwania muhula wa tatu usiokuwa wa kawaida kama kiongozi wa chama.

Mataifa nane ni wanachama wa Shirika la Ushirikianio la Shanghai ikiwemo India na Pakistan.

Iran ni mwangalizi ambaye anatarajiwa kuwa mwanachama kamili katika mkutano huo wa viongozi wakuu.