Mkuu wa WHO: Mwisho wa janga la korona ‘unaonekana’

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus anasema mwisho wa janga la virusi vya korona "unaonekana." Lakini alizitaka nchi kuendelea kuchukua tahadhari.

Tedros aliwaambia wanahabari jana Jumatano kwamba idadi ya vifo vitokanavyo na virusi vya korona duniani kote juma lililopita vilikuwa vya chini zaidi kuripotiwa tangu Machi 2020. Aliendelea kusema kwamba dunia ipo katika nafasi nzuri ya kumaliza janga hilo.

Takwimu za WHO zilionyesha kuwa idadi ya vifo vya kila juma duniani kote kutoka Septemba 5 hadi 11 ilipungua kwa asilimia 22 kutoka juma lililotangulia hadi karibu vifo 11,000.

Shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa, pia liliripoti kuwa visa vipya duniani kote vilipungua kwa asilimia 28 kutoka juma lililotangulia hadi takriban visa milioni 3.13.