Mtaalamu wa Jeshi: Mashambulizi ya kujibu ya Ukraine yanaweza kupungua

Mtaalamu wa kijeshi wa Ukraine anasema mashambulizi ya kujibu yanayoendelea kufanywa na wanajeshi wa nchi yake huenda yakapungua huku vikosi vya Urusi vikisukumwa zaidi mashariki.

Oleksandr Musiienko alikuwa akizungumza hayo katika mahojiano na NHK katika mji mkuu wa Ukraine Kyiv jana Jumatano.

Musiienko alisema mashambulizi ya kujibu ya Ukraine yalisababisha wanajeshi wa Urusi kupoteza nafasi ya kuchukua udhibiti wa eneo la Donbas.

Pia alisema kwamba wanaposonga zaidi mashariki, wanajeshi wa Urusi watakuwa na njia nzuri za usafirishaji kutokea Urusi, na kuongeza kuwa mashambulio ya kujibu ya nchi yake hayatakuwa ya kasi kama ilivyokuwa tangu juma lililopita.

Alipoulizwa kuhusu hatua inayofuata ya vikosi vya Urusi, Musiienko alisema baada ya kuondoka Kharkiv, lengo lao kuu litakuwa kukaa muda mrefu iwezekanavyo kabla ya msimu wa baridi.

Alisema wanajeshi wa Urusi wanafikiri kuwa majira ya baridi yanapokuja, watakuwa na fursa ya kuzitisha nchi za Magharibi kwa nishati na mafuta.

Musiienko aliashiria kwamba kwa kurefusha mapigano, wanajeshi wa Urusi wanangojea "uchovu wa wafadhili" kwa upande wa nchi za Magharibi.