Duru za Habari: Mwenyekiti wa Kadokawa aliomba hitimisho la mapema la ufadhili

Duru za kiuchunguzi zinasema mwenyekiti wa kampuni ya uchapishaji ya Kadokawa ambaye amekamatwa alikutana na mtendaji wa zamani wa kamati ya maandalizi ya Michezo ya Tokyo, Takahashi Haruyuki na kumwomba hitimisho la mapema la mkataba wa ufadhili.

Waendesha mashtaka wa Tokyo walimkamata Kadokawa Tsuguhiko jana Jumatano kwa tuhuma za kumpa rushwa Takahashi.

Waendesha Mashtaka hao wanaamini kuwa Kadokawa alimpatia Takahashi jumla ya yeni milioni 69 au karibu dola 480,000. Fedha hizo zinashukiwa kutolewa kama shukrani kwa Takahashi kwa kufanya mipango ili kampuni hiyo ichaguliwe kama mfadhili wa michezo hiyo.

Kampuni hiyo ilitia saini mkataba na kamati ya maandalizi ya Michezo ya Tokyo mwaka 2019, kisha kuchapisha programu maalum na vitabu vya mwongozo.

Kadokawa amekanusha vikali kumpatia Takahashi rushwa alipozungumza na wanahabari Septemba 5.

Inasemekana Takahashi amekanusha kufanya kosa lolote.