Wakuu wa ulinzi wa Japani na Marekani wakubaliana juu ya suluhu ya amani kwa China na Taiwan

Wakuu wa ulinzi wa Japani na Marekani wamesisitiza tena umuhimu wa amani na utulivu katika Mlango Bahari wa Taiwan huku China ikizidisha shinikizo kwa Taiwan.

Waziri wa Ulinzi wa Japani, Hamada Yasukazu alikutana na Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin katika makao makuu ya wizara ya ulinzi ya Marekani jana Jumatano. Ulikuwa mkutano wao wa kwanza wa ana kwa ana.

Walikubaliana kuzitaka China na Taiwan kutafuta suluhu ya amani.

Hamada alirejelea mapitio ya nyaraka tatu za usalama ikiwamo Mkakati wa Usalama wa Taifa, yanayofanyika hadi kufikia mwishoni mwa mwaka.

Alisema Japani itachunguza chaguzi zote, ikiwa ni pamoja na kile kinachoitwa uwezo wa kujibu mashambulizi, na inataka kimsingi kuimarisha uwezo wake wa ulinzi.

Aliongeza kuwa serikali inalenga kuongeza kwa kiasi kikubwa bajeti ya ulinzi.

Inasemekana Austin alifurahia mawazo hayo.