Nakisi ya biashara nchini Japani yafikia rekodi ya dola bilioni 20

Japani imetoa nakisi ya biashara ya mwezi Agosti ambayo ni rekodi, huku kupanda kwa bei za mafuta ghafi na kudhoofika kwa yeni kukiongeza gharama za bidhaa zinazoingizwa nchini humo.

Wizara ya Fedha ilisema nakisi ya mwezi uliopita ilifikia yeni trilioni 2.82 au takriban dola bilioni 20.

Hiyo ni nakisi kubwa zaidi tangu ulinganishaji wa takwimu ulipoanza kupatikana mwaka 1979. Uwiano wa kibiashara wa Japani umeendelea kuwa hasi kwa miezi 13 mtawalia.

Kiasi cha bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya Japani ziliongezeka kwa karibu asilimia 50 kutoka mwezi sawia mwaka uliotangulia hadi kufikia rekodi ya dola bilioni 76.

Hiyo hasa ilitokana na uagizaji wa mafuta ghafi kuongezeka karibu mara mbili na ule wa gesi asilia ya kimiminika uliongezeka thamani mara 2.4.

Uuzaji bidhaa nje ya nchi uliongezeka kwa asilimia 22 hadi dola bilioni 56.3 kutokana na usafirishaji mkubwa wa magari, mafuta ya dizeli na vifaa vya kuzalisha semikondakta. Hata hivyo ongezeko hilo lilipitwa na ongezeko la zile zilizoingizwa kutoka nje.