Ikulu ya Urusi: Putin kukutana ana kwa ana na Xi kesho Alhamisi

Ofisi ya rais wa Urusi inasema marais Vladimir Putin wa nchi hiyo na Xi Jinping wa China watakutana nchini Uzbekistan kesho Alhamisi.

Ofisi hiyo inasema mkutano wa viongozi hao utafanyika pembezoni mwa mkutano wa viongozi wakuu wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai utakaofanyika katika nchi hiyo.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa viongozi hao wawili kukutana ana kwa ana tangu Urusi ilipoanza uvamizi wake nchini Ukraine mwezi Februari.

Putin anaonekana kuwa na matumaini ya kuthibitisha mahusiano ya kijeshi na kiuchumi na China, katika kipindi ambacho mataifa ya Magharibi yameongeza vikwazo vyake huku jeshi la Urusi linakabiliwa na mashambulizi makali ya kujibu kutoka kwa Ukraine katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.

Ofisi ya rais wa Urusi inasema Putin pia atakutana na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Rais wa Uturuki Recep Tayip Erdogan katika nyakati tofauti kando ya mkutano huo.

Wachambuzi wanasema Putin ana matumaini ya kuimarisha mahusiano na mataifa rafiki katika kipindi ambacho makabiliano yakiendelea na nchi za Magharibi.