Xi anaelekea Asia ya Kati kuhudhuria mkutano wa viongozi wakuu

Rais wa China Xi Jinping anatazamiwa kuzuru Asia ya Kati leo Jumatano kuhudhuria mkutano wa viongozi wakuu wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai ambalo ni mpango kazi wa usalama na uchumi unaoongozwa na China na Urusi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China inasema Xi amepanga kuzuru nchi za Kazakhstan na Uzbekistan kuanzia leo Jumatano hadi Ijumaa.

Hii itakuwa safari ya kwanza ya Xi nje ya China tangu alipotembelea Myanmar mnamo Januari 2020, mwanzoni mwa janga la virusi vya korona.

Jana Jumanne, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning alisema, "Hili litakuwa tukio muhimu zaidi kwa China la kidiplomasia kwa mkuu wa nchi katika mkesha wa Bunge la 20 la Chama cha Kikomunisti cha China."

Wachambuzi wanasema Xi anatarajia kuleta mafanikio ya kidiplomasia kabla ya Bunge la China. Anatarajiwa kutafuta muhula wa tatu ambao haujawahi kushuhudiwa, kama kiongozi wa chama katika bunge.