Kishida kusisitizia umuhimu wa utawala wa sheria katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio anatarajiwa kusisitiza umuhimu wa utawala wa sheria pale atakapotoa hutuba katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York nchini Marekani.

Kishida pia huenda akasisitiza umuhimu wa kuimarisha kazi za Umoja wa Mataifa na kulifanyia mabadiliko Baraza la Usalama.

Atatoa wito huo katika mkutano wa baraza hilo wiki ijayo huku uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ukizidi kuendelea.

Mipango inafanywa kwa Kishida kuhudhuria mkutano wa ngazi ya viongozi wenye lengo la “kujenga kasi ya kuelekea kuwezesha kuingia katika utekelezaji wa Mkataba Unaopiga Marufuku Majaribio ya Nyuklia.”

Maandalizi pia yanafanywa ili Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani Hayashi Yoshimasa aweze kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Hayashi anafikiria kushiriki katika mikutano miwili ya mawaziri wa mambo ya nje, ambayo ni wa Kundi la Nchi Saba zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani na ule wa kundi la Quad. Kundi la Quad linajumuisha Japani, Marekani, Australia na India.