Kikao cha Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa chaiangazia Ukraine

Kikao cha 77 cha Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kimefunguliwa. Nadhari kwa sasa ni kile wajumbe kutoka mataifa wanachama watakochosema kuhusiana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Kikao kilianza jana Jumanne katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, UN jijini New York nchini Marekani.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres alisisitiza kwamba dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile migogoro na umasikini.

Alitoa wito wa amani na mshikamano, akisema dunia inaangazia wajumbe wa mkutano huo kutumia njia zote kwa uwezo wao “kujadili na kufikia muafaka na kupata suluhisho.”

Wawakilishi kutoka mataifa wanachama, wakiwemo viongozi wa serikali na wakuu wa masuala ya kigeni, watatoa hotuba katika mkutano wa baraza hilo kuanzia Jumanne ijayo.

Hotuba hizo zitatolewa ana kwa ana kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka mitatu. Hotuba zilizorekodiwa zilitumika mwaka 2020 na 2021 kutokana na janga la virusi vya korona.