Mfumuko wa bei wa Marekani ulipungua kidogo mwezi Agosti

Wamarekani wanajikuta wakilipa zaidi kwa vitu wanavyohitaji. Wamekuwa wakishuhudia mfumuko wa bei ukiendelea kupanda na walikuwa wakitarajia kupata unafuu. Hata hivyo, hawakupata kabisa kile walichokuwa wakitarajia.

Wizara ya Kazi ilisema kuwa Kipimo cha Bei ya Mlaji kilipanda mwezi Agosti kwa asilimia 8.3 zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Kasi hiyo ilipungua kutoka asilimia 8.5 ya mwezi Julai, lakini bei za bidhaa na huduma nyingi zimefikia rekodi za juu zaidi.

Bei za vyakula zilipanda kwa asilimia 11.4, ikiwa ni kasi ya haraka zaidi katika miaka 43. Japokuwa bei ya petroli imeshuka wakati wote wa majira ya joto, watumiaji bado wanalipa asilimia 25.6 zaidi ya walivyolipa mwaka jana.

Rais Joe Biden wa Marekani alipanga kufanya hafla jana Jumanne ili kusifu kupitishwa kwa sheria ya kupunguza gharama za nishati na huduma za afya.

Hata hivyo, hafla yake ya Sheria ya Kupunguza Mfumuko wa Bei ilinyamazishwa na mfumuko huo wa bei, licha ya kushuka kwa bei za petroli.

Biden alisema, "Tunapiga hatua. Tunapunguza bei zingine pia. Lakini tuna kazi zaidi ya kufanya."

Alikiri kupunguza bei kutachukua "muda zaidi."