WFP yaonya uhaba wa chakula unaweza kuwa mbaya zaidi mwakani

Mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, Kanda ya Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini na Ulaya Mashariki, Corinne Fleischer jana Jumatatu aliiambia NHK kuwa kurejea kwa usafirishaji wa bidhaa za kilimo kutoka Ukraine kulikoathiriwa na vita ni hatua kubwa iliyopigwa.

Hata hivyo Fleischer amesema uvamizi wa Urusi umesababisha uharibifu katika mashamba na miundombinu nchini Ukraine, yakiwemo maeneo ya mashariki ambayo kwa kawaida huzalisha chakula kingi. Pia amesema wakulima wapo mistari ya mbele ya mapambano.

Anatarajia mavuno ya nafaka ya Ukraine kwa msimu ujao kuwa chini kwa karibu asilimia 30 kulinganisha na msimu uliopita, ambao ulishuhudia mavuno mazuri ya tani milioni 100.

Ameonya juu ya uwezekano wa kushuka kwa uzalishaji wa bidhaa za kilimo duniani kutokana na kupanda kwa bei za mbolea baada ya Urusi ambaye ni mzalishaji mkubwa wa bidhaa hiyo kuzuia usafirishaji wa nje.

Pia anatarajia athari mbaya katika usalama wa chakula duniani kutokana na hali za hewa zisizo za kawaida.

Fleischer ameonya kuwa, ikiwa hali hii itaendelea mwakani kunaweza “kusiwe na chakula cha kutosha kulisha dunia.”