Waziri wa mambo ya nje wa Japani alenga kuboresha mahusiano na China

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani Hayashi Yoshimasa ametoa maoni katika ujumbe wa video kwenye kongamano lililofanyika jana Jumatatu. Shirikisho la Makampuni ya Japani ama Keidanren na ubalozi wa China jijini Tokyo walifanya kongamano hilo kabla ya maadhimisho ya miaka 50 ya kurejesha mahusiano ya kidiplomasia mnamo Septemba 29.

Hayashi alisema uhusiano kati ya Japani na China umepiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Alisema biashara za pande mbili zimeongezeka kwa takribani mara 120 zaidi katika kipindi hicho na mabadilishano ya watu yalizidi milioni 12 kabla ya kuenea kwa virusi vya korona.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi pia alihutubia kongamano hilo kwa njia ya video.

Alisema viongozi wa mataifa hayo mawili walifungua ukurasa mpya miaka 50 iliyopita kwa kuondokana na vikwazo kwa ujasiri wa kisiasa na busara pamoja na kuamua kurejesha mahusiano.

Alitoa wito wa kufunguliwa kwa njia ya siku za baadaye ya furaha kwa mataifa hayo mawili na kufanya kazi kuelekea amani na maendeleo.

Pia alisema masuala ya msingi yanayohusiana na Japani na China kama vile Taiwan “yanapaswa kuwa ya wazi.”