Upandikizaji wa seli za iPS kwenye moyo wafanyika jijini Tokyo

Profesa Tabata Minoru wa Chuo Kikuu cha Juntendo jijini Tokyo na Profesa Sawa Yoshiki wa Chuo Kikuu cha Osaka waliwaambia wanahabari jana Jumatatu kuwa jopo la madaktari lilipandikiza karatasi zenye seli za misuli ya moyo kwa mgonjwa mwenye tatizo kubwa la moyo kutofanya kazi.

Karatasi hizo zilitengenezwa kutokana na seli shina za iPS ambazo huundwa kwa kupanga upya seli za mwili wa binadamu na zinaweza kukua na kuwa aina mbalimbali za tishu.

Upasuaji huo uliofanyika mwezi uliopita katika Chuo Kikuu cha Juntendo.

Washiriki wa jopo hilo walisema kwamba mgonjwa huyo aliye katika umri wa miaka ya 60 ameonyesha maendeleo ya kuridhisha na anatarajiwa kuondoka hospitalini hivi karibuni.

Chuo Kikuu cha Osaka kilitengeneza karatasi hizo na kilifanya majaribio ya kitabibu kwa wagonjwa watatu, lakini hii ni mara ya kwanza jaribio hilo limefanyika mahali pengine.

Washiriki hao walisema mara tu matibabu yao yatakapoanzishwa, yatakuwa na ufanisi kwa wagonjwa mahututi ambao matumaini yao pekee ya kuishi ni kwa kupandikiza moyo.