Japani yaidhinisha chanjo ya korona inayolenga Omicron

Japani imeidhinisha matumizi ya chanjo ya virusi vya korona inayolenga virusi hivyo aina ya Omicron kwa watu wenye umri wa miaka 12 ama zaidi ambao wamepata dozi zao mbili za kwanza.

Chanjo yenye valensi mbili iliyotengenezwa na kampuni za dawa za Pfizer na Moderna za Marekani, imebuniwa kulenga aina ya awali ya virusi vya korona na kirusi hicho aina ya Omicron BA.1. Pia inatarajiwa kuwa na ufanisi dhidi ya kirusi kilichopo sasa aina ya BA.5.

Jopo la wataalam katika wizara ya afya jana Jumatatu waliidhinisha matumizi ya chanjo hiyo. Hii inakuja baada ya kampuni za Pfizer na Moderna kuomba idhini ya matumizi mwezi Agosti.

Uamuzi huo utawezesha watu wenye umri wa miaka 12 ama zaidi kupata dozi ya nyongeza ya Pfizer, na wenye miaka 18 ama zaidi kupata dozi ya nyongeza ya Moderna angalau miezi mitano baada ya chanjo ya mwisho.

Wizara hiyo inatarajia watu wapatao milioni 68.5 kuwa na sifa za kupata chanjo hiyo kufikia mwezi ujao.