Uungwaji mkono wa Baraza la Mawaziri la Kishida waporomoka zaidi tangu kuanzishwa kwake

Kura za maoni zilizoendeshwa na NHK zinaonyesha kwamba kiwango cha uungwaji mkono cha Baraza la Mawaziri la Waziri Mkuu Kishida Fumio kimeshuka hadi asilimia 40, kikiwa cha chini zaidi tangu kuundwa kwake mwezi Oktoba mwaka jana.

Kiwango hicho kimepungua kwa alama 6 kutoka utafiti uliofanyika mwezi uliopita. Kiwango cha kutoungwa mkono kimepanda kwa alama 12 hadi asilimia 40.

Miongoni mwa washiriki wanaoliunga mkono baraza hilo, asilimia 42 walisema linaonekana bora kuliko mabaraza mengine, asilimia 25 walisema lina vyama vya siasa wanavyoviunga mkono, na asilimia 17 walisema wanamwamini Kishida.

Kati ya wale wasioliunga mkono baraza hilo, asilimia 36 walisema hawatarajii makubwa kutoka kwenye sera zake, asilimia 29 walisema linakosa uwezo wa kutekeleza sera, na asilimia 12 walisema halina vyama wanavyoviunga mkono.

Kuhusu mazishi ya kitaifa yaliyopangwa Septemba 27 kwa ajili ya Waziri Mkuu wa zamani Abe Shinzo, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi mwezi Julai, asilimia 32 walisema wanakubaliana na hilo, wakati asilimia 57 walisema hawakubaliani.

Walipoulizwa iwapo serikali imeelezea kwa kina juu ya uamuzi wa kufanya mazishi ya kitaifa, asilimia 15 walisema ndiyo wakati asilimia 72 walisema hapana.