Gavana Tamaki wa Okinawa ashinda muhula wa pili

Gavana wa Okinawa, Tamaki Denny ameshinda muhula wa pili katika uchaguzi uliofanyika jana Jumapili.

Tamaki mwenye umri wa miaka 62 alishiriki uchaguzi huo kama mgombea binafsi asiye na chama. Aliungwa mkono na vyama vya upinzani. Mpinzani wake mkuu alikuwa meya wa zamani wa Ginowan, Sakima Atsushi, ambaye aliungwa mkono na muungano unaotawala.

Wakati wa kampeni, Tamaki alisisitiza upinzani wake kwa mpango wa serikali kuu wa kuhamishia Kituo cha Ndege cha Jeshi la Wanamaji la Marekani cha Futenma ndani ya mkoa huo.

Pia alisisitiza mafanikio yake katika muhula wa kwanza, kama vile kushughulikia hali ya umaskini wa watoto.