Modi kuhudhuria mkutano wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai

India imetangaza jana Jumapili kuwa Waziri Mkuu Narendra Modi atahudhuria mkutano wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai.

Mkutano huo wa siku mbili unaohusu mpangokazi wa ushirikiano wa kiusalama na kiuchumi utafanyika mjini Samarkand nchini Uzbekistan kuanzia Alhamisi wiki hii.

Marais Vladimir Putin wa Urusi na Xi Jinping wa China pia wameripotiwa kuhudhuria mkutano huo.

Serikali ya India inasema Modi huenda akafanya mikutano michache ya pande mbili pembezoni mwa mkutano huo.

Huku China ikiongeza shughuli za majini, India inashiriki kwenye mpangokazi wa mataifa manne uitwao “Quad.” Nchi zingine wanachama ni Japani, Marekani na Australia.

Wakati huohuo, India imekuwa ikiepuka kuikosoa moja kwa moja Urusi kwa uvamizi wake nchini Ukraine. Badala yake, imeongeza mno uagizaji wa mafuta ghafi kutoka Urusi.

Macho ya wengi yanataka kuona India itachukua msimamo gani dhidi ya Urusi na China katika mazungumzo hayo yajayo.