Ukraine yaongeza kujibu mashambulizi ili kuchukua udhibiti wa eneo la Kharkiv

Vikosi vya Ukraine vinaongeza kujibu mashambulizi ili kuchukua udhibiti wa maeneo zaidi mashariki mwa Kharkiv, ikiwemo eneo muhimu la kimkakati la Izyum.

Hata hivyo, mtaalamu wa kijeshi wa Ukraine alidokeza kuwa nchi hiyo inahitaji mkakati wa muda mrefu na usaidizi zaidi wa kijeshi kutoka nchi za Magharibi ili kurejesha udhibiti wa maeneo mengi zaidi.

Wizara ya ulinzi ya Urusi ilitangaza juzi Jumamosi kwamba wanajeshi wake watajikusanya tena kutokea mji wa Izyum katika eneo la Kharkiv. Hatua hiyo kwa kiasi kikubwa inapokelewa kama tangazo la kujiondoa katika eneo hilo.

Mkuu wa majeshi ya Ukraine, Jenerali Valerii Zaluzhnyi alituma ujumbe kwenye mtandao wa kijamii jana Jumapili. Alidai kuwa zaidi ya kilomita za mraba 3,000 za eneo zimerudishwa chini ya udhibiti wa Ukraine tangu mwanzoni mwa Septemba.

Naibu Waziri wa Ulinzi wa zamani wa Ukraine Ihor Kabanenko alisema vikosi vya Ukraine vilifanikiwa "kuzuia uwezekano wa wanajeshi wa Urusi kuimarisha vikosi vyao" kwa kudhibiti njia zao za usambazaji. Kabanenko pia alisema "kazi nyingi zaidi" zinahitajika kukomboa maeneo ya Ukraine katika "mkakati wa hatua kwa hatua."