Miaka 21 tangu shambulio la Septemba 11 nchini Marekani

Watu nchini Marekani wamewakumbuka waliokufa katika mashambulio ya kigaidi ya Septemba 11, ambapo watu takriban 3,000 wakiwemo Wajapani 24 waliuawa.

Jamaa wa waathiriwa hao walizuru eneo lililokuwa Kituo cha Kimataifa cha Biashara, WTC jijini New York jana Jumapili, ikiwa ni maadhimisho ya miaka 21 tangu kutokea mashambulio hayo.

Wengi wao waliweka maua na kugusa majina ya wapendwa wao yaliyoandikwa kwenye mnara wa kumbukumbu.

Washiriki wa hafla ya kumbukumbu kwenye eneo hilo walikaa kimya kwa muda. Majina ya waathiriwa yalisomwa kwa sauti.

Magaidi waliziteka ndege nne za abiria mnamo Septemba 11 mwaka 2001. Mbili kati ya hizo ziliruka kuelekea majengo pacha maarufu twin towers ya WTC na nyingine makao makuu ya jeshi la Marekani huko Arlington jimbo la Virginia.

Ndege nyingine ilianguka kwenye uwanja uliopo jirani na mtaa wa Shanksville jimbo la Pennsylvania baada ya usumbufu wa abiria.