Jeneza lililobeba mwili wa Malkia Elizabeth lawasili jijini Edinburgh

Gari lililobeba jeneza lenye mwili wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza limewasili katika jiji la Edinburgh, Scotland.

Msafara huo uliondoka kwenye kasri la Balmoral jana Jumapili, sehemu ambayo Malkia alipenda kukaa msimu wa joto huko Scotland, baada ya kufariki hapo Alhamisi wiki iliyopita akiwa na umri wa miaka 96.

Jeneza lake lilikuwa limefunikwa kwa bendera Maalum ya Kifalme ya Scotland na kupambwa na shada la maua, likiwemo lile alilolipenda likiwekwa juu ya bendera.

Waombolezaji walijipanga ulipopita msafara huo ili kutoa heshima kwa kuwa malkia kwa miaka 70.

Jeneza hilo litahamishwa leo Jumatatu, kutoka Kasri la Holyroodhouse hadi Kanisa Kuu la Mtakatifu Giles jijini humo. Litasalia hapo kwa saa 24 ili kuruhusu wananchi kutoa heshima zao za mwisho.

Baada ya hapo, Jeneza hilo litasafirishwa hadi jijini London kwa ndege ya Jeshi la Anga la Kifalme siku ya kesho Jumanne, kabla ya kuhamishiwa Ukumbi wa Westminster siku inayofuata.

Mwili wa Malkia utasalia hapo kwa siku nne ili kuruhusu umma kutoa heshima zao za mwisho. Mazishi yake ya kitaifa yatafanyika Septemba 19.