Kimbunga Muifa chaelekea taratibu kaskazini karibu na visiwa vya Okinawa

Maafisa wa hali ya hewa nchini Japani wanasema kimbunga Muifa kinasababisha pepo kali na mvua kubwa katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Okinawa kusini mwa Japani.

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini humo inasema hadi kufikia leo Jumatatu mchana kwa saa za Japani, kimbunga hicho kikali kilikuwa karibu na kisiwa cha Ishigaki mkoani Okinawa.

Kimbunga Muifa sasa kina pepo za hadi kilomita 144 kwa saa karibu na kitovu chake na dhoruba ya hadi kilomita 216 kwa saa.

Mamlaka hiyo inatarajia kimbunga Muifa kitaendelea kuelekea kaskazini huku kikisalia na nguvu yake.

Maafisa hao wameeleza kuwa kimbunga hicho kinajongea taratibu. Wanasema hiyo inamaanisha hali mbaya itadumu kwa muda mrefu.

Aidha maafisa hao wanatahadharisha juu ya pepo kali katika eneo la Yaeyama kikiwemo kisiwa cha Ishigaki na eneo jirani la Miyakojima. Pia wanasema mawimbi yanaweza kufika urefu wa mita 10 karibu na maeneo hayo.