Mkuu wa UN atoa wito wa kuipatia msaada Pakistan inayokumbwa na mafuriko

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa dunia kuipatia Pakistan msaada, inayokabiliwa na mafuriko yaliyosababisha uharibifu mkubwa.

Tangu katikati ya mwezi Juni, baadhi ya maeneo ya Pakistan yameshuhudia mvua kubwa zaidi ya wastani wa mvua za mwaka. Mvua hizo zimesababisha mafuriko kwenye maeneo mengi.

Serikali ya Pakistan inasema takribani theluthi moja ya ardhi nchini humo imefunikwa na maji, vifo vya watu 1,396 vimetokea na watu wengine karibu milioni 33 wameathirika.

Serikali inakadiria kwamba uharibifu uliotokea kwenye uchumi na kilimo cha nchi hiyo umesababisha hasara ya zaidi ya dola bilioni 30.

Jana Jumamosi, siku ya pili ya ziara yake nchini humo, Guterres alizuru eneo lililoathirika zaidi kwenye jimbo la kusini la Sindh akiwa na Waziri Mkuu Shehbaz Sharif na maafisa wengine.

Baada ya kuzisikiliza mamlaka za eneo hilo zikimwelezea athari za janga, Guterres alisema, “Ni vigumu kutoguswa pale tunaposikia taarifa za kina za janga.”