Urusi huenda ikajiondoa kutoka katika eneo muhimu la kimkakati mashariki mwa Ukraine

Katika kile kinachoweza kuwa tangazo la kujiondoa lenye ufanisi, wizara ya ulinzi ya Urusi inasema vikosi vyake vitajikusanya tena kutoka kwenye eneo muhimu la kimkakati mashariki mwa Ukraine katika kipindi cha mashambulizi makali ya kujibu mapigo yanayofanywa na vikosi vya Ukraine.

Wizara hiyo jana Jumamosi ilitangaza kuwa vikosi vya Urusi vitajikusanya tena katika maeneo ya Izyum kwenye eneo la Kharkiv ili kuimarisha operesheni zake katika eneo la Donetsk.

Mwanachama mwandamizi wa kundi lililojitenga linaloiunga mkono Urusi katika eneo la Izyum alisema kwamba mabomu yanayopigwa na Ukraine yamefanya hali kuwa mbaya zaidi.

Idara ya usalama ya Ukraine jana Jumamosi ilisema kwamba wanajeshi wa Ukraine walichukua udhibiti tena wa Kupiansk katika eneo la Kharkiv, ambalo lipo katika njia za Urusi za kusambazia bidhaa kwenda kwenye vikosi vilivyopo mstari wa mbele vya Donbas.

Siku hiyo hiyo, Andriy Yermak, mkuu wa Ofisi ya rais Ukraine alituma picha kwenye mtandao wa kijamii zikionyesha vikosi vya Ukraine nje ya Izyum, takribani kilomita 60 kusini mwa Kupiansk.

Izyum inaaminika kuwa kambi muhimu kwa Urusi kupeleka na kuwasilisha bidhaa kwa wanajeshi wake katika eneo la Donbas. Ikiwa Ukraine itachukua udhibiti tena wa Izyum, huenda ikaleta pigo kubwa kwa Urusi.