Kimbunga Muifa kinalikaribia eneo la Okinawa

Maafisa wa mamlaka ya hali ya hewa nchini Japani wameonya kwamba kimbunga kikali kinakaribia mkoa wa Okinawa, kusini mwa nchi hiyo. Wanasema kuwa Kimbunga Muifa kinaweza kusababisha pepo kali na kuchafuka kwa bahari kwenye baadhi ya maeneo.

Mamlaka ya Hali ya Hewa inasema kuwa kimbunga hicho kilikuwa kikielekea kaskazini magharibi katika bahari kusini mwa Okinawa leo Jumapili asubuhi, kwa saa za Japani. Ilisema kuwa kilikuwa kikisafiri kwa kasi ya kilomita 15 kwa saa.

Mamlaka hiyo inatarajia kwamba Kimbunga Muifa kitaendelea kuimarika kikielekea kaskazini magharibi. Mamlaka zinasema inawezekana kimbunga kikavifikia Visiwa vya Sakishima mapema kesho Jumatatu.

Waliongeza kuwa pepo kali huenda zikaanza kulikumba eneo hilo leo Jumapili jioni.

Maafisa wamebainisha kuwa kimbunga kinasogea taratibu. Wanasema hilo linamaanisha hali mbaya zitaweza kudumu kwa muda mrefu zaidi. Pia walisema kwamba mawimbi huenda yakafikia kimo cha mita kumi kwenye maeneo ya Yaeyama na Miyakojima.