Miaka 10 tangu serikali ya Japani inunue baadhi ya visiwa vya Senkaku

Leo Jumapili inatimia miaka 10 tangu serikali ya Japani inunue baadhi ya visiwa vya Senkaku katika mkoa wa Okinawa kutoka kwa mmiliki wa Kijapani.

Serikali ya Japani ilichukua umiliki wa visiwa vitatu vya Senkaku katika Bahari ya China Mashariki mnamo Septemba 11, 2012. Iligusia sababu ya umuhimu wa kuviendeleza na kudumisha visiwa vya Senkaku kwa amani na uthabiti katika kipindi kirefu.

Japani inadhibiti visiwa hivyo. China na Taiwan zinadai umiliki wa visiwa hivyo. Serikali ya Japani inasisitiza kuwa visiwa hivyo ni sehemu ya urithi wa eneo la Japani, kulingana na historia na sheria ya kimataifa. Inasema hakuna suala la uhuru wa kujitawala la kutatuliwa juu ya visiwa hivyo.

China ilijibu vikali juu ya uhamisho wa umiliki huo. Meli za serikali ya China tangu wakati huo mara kwa mara zimeingia katika eneo la bahari la Japani karibu na visiwa hivyo.

Katika miaka ya hivi karibuni, meli za China zimekuwa kubwa na zikiwekwa silaha nzito.

Idadi ya vyombo vya Vikosi vya Kujihami vya Japani kuzuia ndege za China imeongezeka zaidi ya mara nne katika kipindi cha miaka 10. Ndege za kivita za Japani zilizuiwa na zile za China mara 722 katika mwaka wa fedha uliopita ambao ulimalizika mwezi Machi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani Hayashi Yoshimasa aliwaambia wanahabari juzi Ijumaa kuwa hali bado haitabiriki. Aliongeza kuwa serikali inatilia maanani. Hayashi alisema Japani itakuwa macho na kukabiliana na hali kwa utulivu na uthabiti.

Wakati huo huo, Japani na China mnamo Septemba 29 zitaadhimisha miaka 50 ya kurejesha mahusiano ya kidiplomasia.

Mkuu wa Sekratarieti ya Usalama wa Taifa, Akiba Takeo na mwanadiplomasia wa juu wa China Yang Jiechi mwezi uliopita walikubaliana kujaribu kuanzisha mahusiano yenye tija na thabiti.