Dawa za kukabiliana na virusi zaonyesha uwezo wa kukabiliana na Omicron BA.2.75

Watafiti wamesema kuwa dawa nyingi zilizoidhinishwa nchini Japani kwa ajili ya kutibu Ugonjwa wa Virusi vya Korona, COVID-19, zimeonyesha uwezo wa kukabiliana na aina mpya ya kirusi cha korona kiitwacho, Omicron BA.2.75.

Hayo yamebainika katika utafiti uliofanywa na mkuu wa jopo la utafiti, Profesa Kawaoka Yoshihiro, wa Taasisi ya Sayansi za Tiba katika Chuo Kikuu cha Tokyo na wanasayansi wengine 13 wa Japani na Marekani, ambao matokeo yake yamechapishwa kwenye jarida la ‘New England Journal of Medicine’.

Watafiti hao wamesema kuwa, dawa aina ya remdesivir, molnupiravir na nirmatrelvir zinazotumika kukabiliana na virusi huenda zikawa na uwezo wa kukabiliana na aina mpya ya kirusi cha korona kiitwacho, Omicron BA.2.75 kilichobainika kwenye nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Marekani, Uingereza na Japani.

Dawa aina ya casirivimab-imdevimab na sotrovimab ambazo huzalisha kinga za kufifisha makali ya kirusi, zimeonekana kuwa na uwezo mdogo zaidi wa kukabiliana na aina hiyo mpya ya kirusi cha korona.

Hata hivyo, watafiti hao wamesema kuwa, dawa aina ya tixagevimab- cilgavimab ambayo iliidhinishwa kwa matumizi ya kukabiliana na virusi vya korona mwezi uliopita, imeonyesha uwezo mkubwa wa kukabiliana na virusi hivyo.