Nchi wanachama wa IPEF zakubaliana kuanza majadiliano, India haitahusika majadiliano ya kibiashara

Mawaziri wa biashara kutoka Japani, Marekani na mataifa mengine 12 wamekubaliana kuanza rasmi majadiliano kuhusu mkakati mpya wa kiuchumi kwa eneo la Indo-Pasifiki.

Makubaliano hayo yalifikiwa jana Ijumaa wakati mawaziri hao wakihitimisha mkutano wa kwanza wa ana kwa ana kuhusu Mpango-mkakati wa Kiuchumi kwa Ustawi wa eneo la Indo-Pasifiki, maarufu kama ‘IPEF’, uliofanyika jijini Los Angeles, nchini Marekani.

Mwakilishi wa masuala ya biashara kutoka Marekani, Katherine Tai, na Waziri wa Biashara, Gina Raimondo, walitoa taarifa hiyo kwenye mkutano wao na waandishi wa habari.

Tai alisema, “Mkutano huu ulikuwa ni nafasi ya kuimarisha zaidi ushirikiano wetu na kuweka taarifa za kina kuhusu namna tutakavyoshirikiana katika kushughulikia changamoto na fursa zitakazotoa mwelekeo wa karne ya 21.”

Mataifa 14 wanachama wa IPEF yanazijumuisha pia India na Australia.

Kufanya biashara kwa njia za kidijitali pamoja na kuimarisha njia za usambazaji wa bidhaa muhimu kama vile ‘sakiti changamano’, ni miongoni mwa mambo makuu manne yanayojadiliwa.

Nchi wanachama zinaweza kuchagua maeneo ya kujiunga katika mkakati huo wa IPEF. India imechagua kutoshiriki majadiliano ya kibiashara, lakini mataifa mengine yanaendelea na majadiliano katika maeneo yote manne.

Waziri wa Uchumi, Biashara na Viwanda wa Japani, Nishimura Yasutoshi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa anataka kuanzisha majadiliano hayo mapema iwezekanavyo.