Putin akosoa vikwazo vya nchi za Magharibi

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amekosoa vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi ambavyo vinakwamisha mauzo ya nje ya mbolea ya Urusi kwenda mataifa ya Afrika, Asia na Amerika Kusini.

Putin aliyasema hayo jana Ijumaa wakati akizungumza kwenye mkutano wa usalama uliofanyika katika ofisi ya rais jijini Moscow.

Alivielezea vikwazo vilivyowekwa kufuatia uvamizi wa kijeshi unaofanywa na Urusi nchini Ukraine kama ‘ubaguzi’.

Alisema kuwa, mauzo ya nje ya nafaka kutoka Ukraine yamerejea kwenye hali ya kawaida, lakini kiasi kikubwa kimesafirishwa kwenda Barani Ulaya na sio kwenye mataifa masikini zaidi.

Rais Putin anatarajia kukutana na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan juma lijalo ambapo atatoa pendekezo la kuweka ukomo wa mauzo ya bidhaa za kilimo kwenda mataifa ya Ulaya.

Uturuki, kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, iliratibu makubaliano baina ya Ukraine na Urusi yaliyolenga kurejesha mauzo ya nje ya nafaka kutoka nchini Ukraine.