IAEA: Hali katika mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia si thabiti

Wakaguzi kwenye mtambo mkubwa zaidi wa nyuklia Barani Ulaya wanaonya juu ya uwezekano wa kutokea janga kubwa. Wamesema ukataji wa umeme na mashambulizi ya kijeshi kwenye maeneo ya mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia nchini Ukraine kunasababisha mazingira ya kukosekana kwa “uthabiti.”

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA, Rafael Grossi alituma picha ya video inayoonyesha hali hiyo, jana Ijumaa.

Alisema, “Mtambo wa nishati ya nyuklia hauwezi kugeuzwa kuwa mateka wa kivita. Hatma yake kamwe haipaswi kuamuliwa kwa njia za kijeshi. Athari za vitendo kama hivyo ni mbaya sana.

Grossi alitoa wito wa kukomeshwa haraka mashambulizi yote ya mabomu kwenye eneo lote la mtambo huo. Alirejelea wito wake kwa kuanzishwa ukanda wa usalama wa nyuklia.

Umeme wa gridi ya taifa ulikatwa kwenye mtambo huo Jumatatu iliyopita, na tangu wakati huo mafundi wamekuwa wakitegemea kinu kimoja pekee kinachofanya kazi katika kuhakikisha mifumo ya usalama kwenye mtambo huo inaendelea kufanya kazi. Hata hivyo, wanatafakari juu ya mpango wa kuzima kinu hicho na kuendesha mtambo huo kwa majenereta yanayotumia mafuta ya diseli.