Mfalme wa Japani atoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Malkia wa Uingereza

Mfalme Naruhito wa Japani ametoa taarifa inayoelezea masikitiko yake makubwa na salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza.

Katika taarifa yake Mfalme Naruhito alisema angependa kuelezea heshima na shukurani zake za dhati kwa maisha ya Malkia, mafanikio yake na kujitolea kwake.

Familia ya Mfalme wa Japani imekuwa na uhusiano wa karibu wa muda mrefu na Familia ya Malkia wa Uingereza.

Mfalme wa zamani wa Japani, Akihito, alihudhuria hafla ya kutawazwa malkia wa Uingereza mwaka 1953, kwa niaba ya Mfalme Showa. Kwenye miaka ya 1980, Mfalme Naruhito alisoma kwenye Chuo Kikuu cha Oxford na tangu wakati huo amezuru rasmi nchini humo mara tatu na kula pamoja na Malkia.

Kwenye taarifa yake, Mfalme alibainisha kwamba mara zote Malkia alikuwa na mtazamo chanya kuhusu uhusiano baina ya nchi hizo mbili, na kutilia maanani uhusiano kati ya familia ya Malkia wa Uingereza na familia ya Mfalme wa Japani.

Mfalme alielezea shukrani zake za dhati kwa namna Malkia alivyomjali wakati alipokuwa mwanafunzi kwenye Chuo Kikuu cha Oxford, na pia wakati alipofanya ziara nchini Uingereza.