Waombolezaji wajikusanya Kasri ya Buckingham kumuenzi Malkia Elizabeth

Rambirambi zinazidi kutolewa kufuatia kifo cha malkia aliyeitawala Uingereza kwa muda mrefu zaidi. Malkia Elizabeth wa Pili alitawala kwa miaka 70 hadi alipofariki dunia juzi Alhamisi akiwa na umri wa miaka 96.

Watu wengi walikusanyika kwenye Kasri ya Buckingham jijini London nchini Uingereza jana Ijumaa na kuelezea kushtushwa na taarifa za kifo cha malkia.

Malkia Elizabeth wa Pili amerithiwa na mwanae mkubwa, Mfalme Charles wa Tatu, ambapo kufuatia mabadiliko hayo, sarafu na wimbo wa taifa wa Uingereza vitabadilishwa pia.

Wimbo wa taifa wa Uingereza sasa utakuwa “Mungu Mlinde Mfalme,” badala ya “Mungu Mlinde Malkia.” Malkia Elizabeth wa Pili alitawala kwa miongo saba na mara nyingi alikuwa akiitwa “mwamba” wa Uingereza.

Ibada ya Mazishi ya kitaifa inatarajiwa kufanyika katika kanisa la Westminster Abbey jijini London ndani ya majuma mawili. Kabla ya hapo, mwili wa Malkia utakuwa kwenye ikulu ya nchi hiyo kwa siku nne ambapo waombolezaji watapata fursa ya kutoa heshima za mwisho.