Afisa wa Wizara ya Fedha asema Japani iko tayari kuchukua hatua dhidi ya kushuka kwa yen

Afisa mwandamizi wa Wizara ya Fedha ya Japani ametoa onyo kuhusu kasi ya kushuka thamani ya sarafu ya yen. Hayo yametokea wakati sarafu ya Japani ikifikia kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka 24 dhidi ya dola.

Afisa huyo anasema kushuka huko kwa hivi karibuni hakuwezi kuhusishwa tu na mambo ya misingi na kwamba serikali na Benki ya Japani wana wasiwasi mkubwa.

Naibu Waziri wa Fedha wa Masuala ya Kimataifa wa Japani, Kanda Masato alisema, “Iwapo yen itaendelea na mwendo huu, tuko tayari kuchukua hatua zinazohitajika katika soko la sarafu. Tutafanya lolote liwezekanalo.”

Kanda alitoa ufafanuzi huo baada ya mkutano na maafisa kutoka Idara ya Huduma za Fedha na Benki ya Japani.

Maafisa hao walithibitisha kuwa watafuatilia kwa karibu athari za kasi ya kushuka kwa thamani ya yen kwa uchumi wa Japani na bei za bidhaa.