Blinken azuru Ukraine katika ‘wakati muhimu’

Viongozi wa Ukraine wameviona vikosi vyao vikiongeza kujibu mashambulizi na kutwaa tena eneo ambalo walihofia kuwa walilipoteza. Walifanya mashambulizi kwa msaada wa silaha kutoka nchi za Magharibi. Na sasa wanakaribia kupata silaha zaidi.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskky alimkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken jijini Kyiv jana Alhamisi. Blinken anaamini kwamba vita hivyo vinaweza kuwa katika hatua ya mabadiliko.

Blinken alisema “Tunajua huu ni wakati muhimu. Zaidi ya miezi sita ya vita ya uchokozi wa Urusi dhidi ya Ukraine, huku kujibu kwako mashambulizi kukiendelea na kuonyesha ufanisi.”

Blinken alitangaza msaada wa kijeshi wenye thamani ya dola bilioni 2.8 kwa ajili ya Ukraine na nchi nyingine 18 zilizo katika hatari ya tishio la Urusi.

Maafisa kutoka Wizara ya Ulinzi ya Marekani na washirika wao walikusanyika katika kambi ya jeshi la anga iliyopo Ujerumani ili kuratibu usambazaji wa msaada huo. Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin alisema sura ya vita inabadilika lakini akaapa watafanya kazi pamoja “kwa muda mrefu.”