Viongozi wa nchi 8 wakubaliana kushirikiana kushughulikia hali nchini Ukraine

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio, Rais wa Marekani Joe Biden na viongozi wa baadhi ya nchi nyingine wamesisitiza tena kwamba watashirikiana kukabiliana na hali iliyopo nchini Ukraine.

Mkutano kwa njia ya video uliohimizwa na Biden ulifanyika jana Alhamisi jioni, kwa saa za Japani. Mkutano huo ulidumu kwa takribani saa moja. Viongozi wa nchi nane walishiriki. Wakuu wa baadhi ya nchi wanachama wa G7 walikuwa miongoni mwa washiriki. Lakini Rais wa Ufaransa hakushiriki.

Viongozi hao walibadilishana mawazo kuhusu hali nchini Ukraine. Walikubali kuendelea kuiunga mkono nchi hiyo na kudumisha vikwazo vikali dhidi ya Urusi.

Pia walikubaliana kwamba nchi zao zinapaswa kufanya kazi pamoja kwa ukaribu ili kuhakikisha usambazaji thabiti wa nishati na chakula.

Kishida alizungumza kuhusu hatua za hivi karibuni za Urusi katika eneo la Indo-Pasifiki. Alisisitiza kwamba ni muhimu kuzifikia nchi ambazo zimechukua msimamo wa kutoegemea upande wowote.

Aidha Kishida aliitaja Mkutano wa Nane wa Kinataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika. Mkutano huo ulifanyika nchini Tunisia mwezi uliopita. Kishida alisema wawakilishi wa mataifa yaliyoshiriki walielezea wasiwasi wao kuhusu uchokozi wa kijeshi wa Urusi.