Viongozi duniani watuma salamu za rambirambi

Mwana wa kiume wa Malkia Elizabeth, Charles ambaye kwa muda mrefu amekuwa mrithi wa kiti cha ufalme, sasa ndiye mfalme. Alitoa taarifa jana Alhamisi juu ya kifo cha “mama yake kipenzi.”

Alisema ni kipindi cha “huzuni kubwa” kwa familia yake lakini watafarijiwa kwa kuelewa “heshima na upendo wa dhati aliokuwa nao Malkia kwa kiasi kikubwa.”

Waziri Mkuu Liz Truss alimsifia Malkia kuwa “Ni ari ya Uingereza,” na kuongeza kuwa alikuwa msingi ulioijenga Uingereza ya sasa na kwamba nchi imekuwa na kustawi chini ya utawala wake.

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio pia alielezea rambirambi zake. Kishida alisema Malkia alifanya jukumu la kipekee la kudumisha amani ya dunia na ustawi, na inakuwa ni hasara kubwa siyo kwa watu wa Uingereza, lakini pia kwa jumuiya ya kimataifa. Alisema Japani itakuwa pamoja na watu wa Uingereza katika kuishinda huzuni hii kubwa.

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau alisema neema halisi na azimio lake limeleta faraja na nguvu kwa kila mtu “katika dunia yenye utata.” Kiongozi huyo wa taifa kubwa la Jumuiya ya Madola alisema huduma ya Malkia kwa watu wa Canada itabaki kuwa sehemu muhimu kwenye historia yao.