Malkia Elizabeth wa II afariki akiwa na umri wa miaka 96

Malkia Elizabeth wa Uingereza aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi wa miaka 70 amefariki dunia. Alikuwa na umri wa miaka 96.

Malkia huyo alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kiafya kwa takriban miezi kadhaa.

Lakini katika siku za hivi karibuni, daktari wake alizidi kutilia shaka juu ya hali yake ya kiafya. Hali hiyo iliwafanya wanafamilia ya kifalme kuungana naye haraka katika makazi yake yaliyopo Scotland.

Mwanamfalme Charles ambaye ndiye mrithi wa kiti cha ufalme, mkewe Camilla na mwanamfalme William walikuwa ni miongoni mwa waliofika katika kasri la Balmoral.

Mapema wiki hii, Malkia Elizabeth alikutana na Waziri Mkuu mpya Liz Truss kumthibitisha rasmi katika wadhifa wake, hafla ya kitamaduni ambayo malikia amekuwa akiifanya kwa miongo kadhaa.

Baadaye alilazimika kufuta mkutano wake kwa njia ya mtandao na Baraza la Siri juzi Jumatano, chombo ambacho humpa ushauri.

Hali ya kiafya ya Malkia ilimfanya afute kazi nyingi zinazomfanya aonekane kwa umma.

Mara nyingi alibaki katika kasri la Windsor, makazi yake yaliyo nje ya jiji la London.

Lakini aliendelea na utaratibu wake wa majira ya joto wa kurejea katika kasri la Balmoral lililopo Scotland, moja ya sehemu anayoipenda zaidi.

Malkia Elizabeth alifariki dunia akiwa katika kasri hilo jana Alhamisi mchana.