Kipimo cha bei ya mafuta chashuka kiwango cha chini kwa miezi 8

Hofu ya kupungua kwa kasi ya ukuaji uchumi duniani imefanya kipimo cha bei za mafuta ghafi nchini Marekani kushuka kwa kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miezi minane.

Kipimo cha WTI kilimaliza kikiwa chini ya dola 82 kwa pipa moja jana Jumatano. Hicho ni kiwango cha chini zaidi tangu katikati ya mwezi Januari.

Kipimo hicho kilishuka kwa vile vizuizi vya virusi vya korona nchini China vinachelewesha urejeshaji wa mahitaji ya mafuta.

Wasiwasi kuhusu athari kubwa ya kupungua kasi ya ukuaji uchumi pia unaongezeka kwa kuwa benki kuu za Marekani na Ulaya zinapandisha viwango vya riba kwa lengo la kudhibiti mfumko wa bei.