Putin kukutana ana kwa ana na Xi Jinping juma lijalo

Rais wa Urusi Vladimir Putin amethibitisha mipango ya kukutana na rais wa China Xi Jinping nchini Uzbekistan juma lijalo.

Uthibitisho huo ulikuja wakati wa mkutano wake jana Jumatano na Li Zhanshu ambaye ni mwenyekiti wa Kamati Kuu ya bunge la China.

Li alihudhuria Kongamano la Uchumi la Mashariki huko Vladivostok, ambapo Putin alitoa hotuba.

Ofisi ya rais wa Urusi ilisema Putin alimkaribisha afisa huyo wa ngazi ya tatu wa serikali ya China, akisema ziara ya Li "inaonyesha hali maalum ya uhusiano wa Urusi na China."

Putin pia alielezea matumaini ya kukutana na Rais Xi hivi karibuni.

Alisema atafanya mazungumzo na Xi wakati wa mkutano wa siku mbili wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai nchini Uzbekistan utakaoanza Septemba 15.

Putin pia alifichua mipango ya kufanya mazungumzo ya pande tatu na Rais wa Mongolia Ukhnaa Khurelsukh katika tukio hilo nchini Uzbekistan.