Jopo la wataalam la Marekani: Ukraine huenda imevirudisha nyuma vikosi vya Urusi mjini Kharkiv

Taasisi ya Utafiti wa Vita ya wataalam wa Marekani inasema vikosi vya Ukraine vilianza kujibu mashambulizi juzi Jumanne katika jimbo la mashariki la Kharkiv ambayo huenda yalivirudisha nyuma vikosi vya Urusi.

Iliongeza kuwa kuondolewa kwa vikosi vya Urusi kutoka Kharkiv na mashariki mwa Ukraine kwenda kusini huenda kumeipa fursa Ukraine ya kujibu mashambulizi.

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema jana Jumatano kwamba juhudi kuu zilizopangwa za Urusi labda ni kusonga mbele katika jiji la Bakhmut lililopo eneo la mashariki la Donbas.

Lakini wizara hiyo ilisema kwamba makamanda wa Urusi wanakabiliwa na mkanganyiko wa kupeleka akiba ya wanajeshi kusaidia mashambulizi hayo au kujilinda dhidi ya Ukraine inayosonga mbele eneo la kusini.

Mkuu wa Jeshi la Ukraine alitangaza jana Jumatano kwamba karibu ngome kuu 40 za jeshi la Urusi zilishambuliwa.