Mkuu wa chekechea aomba radhi kufuatia kifo cha mtoto wa miaka 3

Mkuu wa shule moja ya chekechea mkoani Shizuoka uliopo katikati mwa Japani, ameomba radhi kufuatia kifo cha binti mwenye umri wa miaka mitatu aliyeachwa ndani ya basi la shule.

Kawamoto China alifariki kwa ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto kali baada ya kuachwa kwa takriban saa tano ndani ya basi katika shule ya chekechea ya Kawasaki mjini Makinohara Jumatatu wiki hii.

Mkuu wa shule hiyo Masuda Tatsuyoshi na makamu mkuu wa shule Sugimoto Tomoko walizungumza na wanahabari jana Jumatano.

Mkuu wa shule aliashiria kujiuzulu wadhifa wake mara baada ya mrithi wake kupatikana.

Mkuu huyo wa shule aliendesha basi hilo siku ya tukio kwa kuwa dereva wa kawaida alichukua mapumziko ya siku ghafla. Alikiri kwamba alishindwa kuhakikisha kuwa watoto wote wameshuka kwenye basi hilo kwa vile hakuwa mzoefu wa kazi hiyo.

Naye makamu mkuu wa shule alielezea kwamba hakukuwa na sheria iliyotaka mfanyakazi zaidi ya mmoja kukagua ikiwa kuna mtoto yeyote ameachwa ndani ya basi.

Pia alisema mwalimu wa darasa alilokuwa akisoma binti huyo alidhani mtoto huyo hakuwa darasani kwa kuwa hakuhudhuria shule kutokana na sababu fulani, na hakuthibitisha kwa wazazi wake wala walimu wengine.