Japani yalegeza vizuizi vya matembezi kwa wagonjwa wa korona

Waziri wa afya wa Japani Kato Katsunobu ametangaza kuwa serikali sasa inaruhusu wagonjwa wa virusi vya korona wasio na dalili kufanya matembezi muhimu ikiwa watazingatia hatua za kuzuia virusi.

Waziri huyo alikutana na wanahabari jana Jumatano jioni.

Alisema vizuizi vya matembezi kwa wagonjwa wa korona wanaojiuguza majumbani vimepunguzwa kwa wasiokuwa na dalili za ugonjwa huo na wale ambao dalili zao zimeshuka kwa saa 24.

Aliongeza kuwa watu hao bado watahitajika kuchukua hatua za hiyari kuzuia maambukizi, ikiwemo kuvaa barakoa, lakini hawatalazimika tena kujiepusha na matembezi muhimu, kama vile kununua chakula.

Juzi Jumanne serikali iliamua kufupisha muda wa kujitenga kwa wagonjwa wenye dalili za korona kutoka kiwango cha chini cha sasa cha siku 10 hadi saba. Vilevile kipindi cha wagonjwa wasio na dalili kitapunguzwa kutoka siku saba za sasa hadi tano.