Marekani: Urusi yajaribu kununua vifaa vya kijeshi kutoka Iran na Korea Kaskazini

Serikali ya Marekani inaashiria kwamba Urusi inaelekea kununua silaha kutoka Iran na Korea Kaskazini kwa kuwa imepata hasara kubwa ya vifaa vya kijeshi na maafisa katika uvamizi wake nchini Ukraine.

Vikosi vya Ukraine vinaendelea kujibu mashambulizi katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo ikiwemo Kherson. Jeshi la nchi hiyo linasema vikosi vyake vimechukua tena maeneo kadhaa kusini na mashariki mwa nchi hiyo.

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza jana Jumanne ilisema kwamba idadi ya mashambulizi yaliyoripotiwa ya ndege zisizokuwa na rubani za Urusi katika eneo la kusini la Kherson yalikuwa machache kuliko mwezi Agosti.

Wizara hiyo iligusia upungufu wa idadi ya droni ulisababishwa na vikwazo vya kimataifa. Wizara hiyo iliongeza kuwa upungufu huo ulikuwa unatatiza operesheni za jeshi la Urusi.

Serikali ya Marekani, wakati huohuo imeelezea wasiwasi kwamba Iran inashughulikia kuipatia Urusi mamia ya droni.

Afisa mwandamizi wa Ikulu ya Marekani pia alisema jana Jumanne kuwa Urusi inajaribu kununua mamilioni ya mizinga na roketi kutoka Korea Kaskazini kwa ajili ya vita nchini Ukraine.