Mshirika anayeshukiwa: ‘Malipo ya Kadokawa yalikuwa zawadi ya ufadhili’

Mkuu wa kampuni iliyopokea malipo kutoka kwa mchapishaji wa Kijapani Kadokawa aliripotiwa kusema alidhani pesa hizo zilikuwa zawadi ya kupokea mkataba wa kufadhili Michezo ya Olimpiki na Paralimpiki ya Tokyo.

Fukami Kazumasa alikamatwa na wapelelezi jana Jumanne. Anashukiwa kuhudumu kama mshirika wa mtendaji wa zamani wa kamati ya maandalizi ya Michezo ya Tokyo, Takahashi Haruyuki.

Takahashi alikamatwa tena siku hiyo hiyo. Anashukiwa kupokea rushwa kutoka kwa maafisa wakuu wa zamani wa Kadokawa.

Mtendaji mkuu wa zamani wa Kadokawa, Yoshihara Toshiyuki, na afisa mwandamizi wa zamani, Maniwa Kyoji, walikamatwa kwa kutoa rushwa hiyo.

Wanashukiwa kumlipa Takahashi jumla ya yen milioni 69, ama takriban dola 480,000, kuiwezesha kampuni hiyo kuchaguliwa kama mfadhili wa Michezo ya Tokyo.