Serikali ya Japani yatafakari kutoa fedha kwa ajili ya familia zinazotaabika na ongezeko la bei

Serikali ya Japani inafikiria kutoa fedha yen 50,000 ama takriban dola 350 kwa kila familia yenye kipato cha chini ili kuzisaidia kukabiliana na kupanda kwa bei ya nishati na vyakula.

Hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa Waziri Mkuu Kishida Fumio wa kuendelea kusaidia kampuni na familia zinazotaabika kutokana na kupanda kwa bei kulikosababishwa kwa kiasi kikubwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Serikali inapanga kutoa fedha hizo kwa familia ambazo zimesamehewa kodi ya wakaazi. Inakusudia kufadhili mpango huo ambao huenda ukagharimu zaidi ya dola bilioni 6 kwa kutumia fedha za akiba za bajeti ya mwaka huu wa fedha.

Serikali inafanya mipango ya mwisho na vyama tawala ili kutekeleza utoaji wa fedha hizo. Maafisa wanatumai kuwa fedha hizo zitaidhinishwa mapema siku ya Ijumaa wiki hii katika mkutano wa kikosi kazi cha serikali.