Yen yashuka hadi 144 kwa dola

Yen inaendelea kushuka, wakati mmoja ikishuka hadi kiwango cha yen 144 kwa dola leo Jumatano. Kiwango hicho ndio dhaifu zaidi kuwahi kutokea tangu Agosti 1998. Sarafu hiyo ya Japani imeshuka kwa takriban yen 7 katika siku 10 zilizopita za biashara.

Kushuka kwa thamani kunakuja baada ya vipimo vya shughuli za kampuni zisizozalisha nchini Marekani kutangazwa kuwa vikubwa kuliko ilivyotarajiwa jana Jumanne.

Faida ya dhamana ya Marekani ya miaka kumi ilipanda hadi zaidi ya asilimia 3.3 kufuatia tangazo hilo, kiwango cha juu zaidi tangu Juni 16.

Wabobezi wa soko wanaamini kuwa Benki Kuu ya Marekani itaendelea kuongeza viwango vya riba, licha ya hatari ya kupoza uchumi.

Kuongezeka kwa pengo la viwango vya riba kati ya Japani na Marekani kumesababisha wafanyabiashara kuuza yen zao ili kutafuta faida ya juu zaidi ya dola.

Kushuka kwa thamani ya yen kumeongezeka kwa kasi tangu Mwenyekiti wa Benki Kuu ya Marekani Jerome Powell aliposema wazi katika hotuba mnamo Agosti 26 angeendelea kuongeza viwango vya riba. Wakati huo huo, Benki ya Japani imeonyesha kuwa inapanga kuendelea na sera zake za kulegeza hatua zake kubwa.

Wachambuzi wanasema wanatarajia uuzaji wa yen utaendelea kwa muda mrefu kama viwango vya riba vitaendelea kuwa chini nchini Japani.